Deuteronomy 17

1 aMsimtolee Bwana Mwenyezi Mungu wenu dhabihu ya maksai au kondoo ambaye ana dosari yoyote au hitilafu ndani yake, kwa kuwa hilo litakuwa chukizo kwake.

2 bIkiwa mwanaume au mwanamke anayeishi kati ya mojawapo ya miji akupayo Bwana, anakutwa anafanya uovu mbele za Bwana Mwenyezi Mungu wenu, kwa kuvunja Agano lake, 3 cnaye amekwenda kinyume na agizo langu kuabudu miungu mingine na kuisujudia, kama vile jua, mwezi au nyota za angani, 4 dhili likiwa limeletwa mbele yenu, ni lazima kulichunguza kikamilifu. Ikiwa ni kweli na kuwa limehakikishwa kwamba hili ni chukizo lililofanyika katika Israeli, 5 emchukueni huyo mwanaume au mwanamke ambaye amelifanya tendo hili ovu kwenye lango la mji wenu na kumpiga mawe mtu huyo mpaka afe. 6 f gKwa ushuhuda wa mashahidi wawili au watatu mtu huyo atauawa, bali hakuna mtu atakayeuawa kwa ushuhuda wa shahidi mmoja tu. 7 hNi lazima kwanza mikono ya mashahidi itangulie kumuua huyo mtu, kisha mikono ya watu wote. Ni lazima mwondoe uovu miongoni mwenu.

Mahakama Za Sheria

8 iKama mashauri yanaletwa katika mahakama zenu ambayo ni magumu zaidi kwenu kuyaamua, ikiwa ni umwagaji wa damu, madai au mashambulio, yapelekeni mahali ambapo Bwana Mwenyezi Mungu wenu atapachagua. 9 jNendeni kwa makuhani, ambao ni Walawi, na kwa mwamuzi ambaye atakuwa kazini wakati huo. Ulizeni kwao nao watawapa maamuzi. 10Ni lazima mtende sawasawa na maamuzi watakayowapa mahali Bwana atakapopachagua. Kuweni waangalifu kufanya kila kitu watakachowaongoza kufanya. 11 kFanyeni sawasawa na sheria wanayowafundisha na maamuzi wanayowapa. Msigeuke mkono wa kuume au kushoto kuacha kufanya yale wanayowaambia. 12 lMwanaume atakayeonyesha dharau kwa mwamuzi au kwa kuhani ambaye amewekwa kumtumikia Bwana Mwenyezi Mungu wenu lazima auawe. Lazima mwondoe uovu katika Israeli. 13 mWatu wote watasikia na kuogopa, nao hawatakuwa wenye kudharau tena.

Mfalme

14 nWakati utakapoingia katika nchi anayowapa Bwana Mwenyezi Mungu wenu kuimiliki na kukaa humo, nanyi mkasema, “Na tumweke mfalme juu yetu kama mataifa yanayotuzunguka,” 15 okuweni na uhakika wa kumweka mfalme juu yenu ambaye Bwana Mwenyezi Mungu wenu atamchagua. Ni lazima atoke miongoni mwa ndugu zenu wenyewe. Msimweke mgeni juu yenu ambaye si ndugu wa Kiisraeli. 16 pHata hivyo, kamwe mfalme asijipatie hesabu kubwa ya farasi kwa ajili yake mwenyewe, au kuwafanya watu warudi Misri ili kupata farasi zaidi, kwa maana Bwana amekuambia, “Hamtairudia njia ile tena.” 17 qKamwe asioe wake wengi, la sivyo moyo wake utapotoka. Kamwe asijilimbikizie kiasi kikubwa cha fedha na dhahabu.

18 rAtakapokuwa amekalia kiti cha ufalme wake, ajiandikie kwenye kitabu nakala ya sheria kwa ajili yake mwenyewe kutoka zile sheria za makuhani ambao ni Walawi. 19 sAtakuwa na nakala hiyo, naye ataisoma siku zote za maisha yake ili kwamba ajifunze kumheshimu Bwana Mwenyezi Mungu wake na kufuata kwa uangalifu maneno yote ya sheria hii na amri hizi, 20 tnaye asijifikirie kuwa ni bora kuliko ndugu zake na kuipotosha sheria. Ndipo yeye na wazao wake watatawala katika ufalme wake kwa muda mrefu katika Israeli.
Copyright information for SwhKC